Jumatatu, tarehe 8 Julai 2025, kampuni inayozalisha mbolea ya kikaboni na ya madini, FOMI, ilipokea wageni kutoka nchini Tanzania. Walikuwa wakiongozwa na mkuu wa taasisi ya udhibiti wa mbolea nchini Tanzania, Tanzania Fertilizer Regulatory Authority, Dkt. Antony Diallo.
Katika hotuba yake ya ukaribisho, Mkurugenzi Mkuu wa FOMI, Simon Ntirampeba, aliwapatia ufupisho wa historia ya kiwanda.
Mkurugenzi Mkuu alieleza jinsi wanavyofanya kazi pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Mazingira katika kuwasaidia wakulima kupata mbolea.
Alisema kuwa Serikali ndiyo inawaalika wakulima kujiandikisha, na baadaye kulipia kiasi cha mbolea kulingana na kiwango na aina wanayoihitaji.
Alieleza pia kuwa malori ya FOMI ndiyo husambaza mbolea hadi katika maeneo mbalimbali nchini ili wakulima wapate mbolea karibu na maeneo yao.
Baadhi ya wageni walitoa maswali, wakitaka kujua ikiwa mbolea inayozalishwa na FOMI inatosha kuwahudumia wakulima wote, na kama kuna viwanda vingine vinavyozalisha mbolea mbali na FOMI.
Mkurugenzi Mkuu alijibu maswali hayo mbalimbali.
Dkt. Antony Diallo, aliyekuwa akiongoza ujumbe huo, alisema kuwa walikuja kupata ujuzi ili waweze kujifunza mbinu za kushirikiana na kiwanda cha ITRACOM Fertilizer katika kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa urahisi.
Alieleza kuwa wamejifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kazi ya kusambaza mbolea kwa wananchi.
Aliwapongeza viongozi wa FOMI kwa jinsi wanavyoshirikiana na wizara pamoja na benki katika juhudi za kuwasogezea mbolea wananchi.